Dar es Salaam. Wakati Yanga wakishuka dimbani leo kucheza mechi
ya kirafiki dhidi ya timu ya Pillars ya Nigeria, uongozi wa klabu hiyo,
umeitisha mkutano wa dharura kujadili udhamini wa kituo cha Televisheni
cha Azam.
Yanga ndiyo klabu pekee kati ya 14 zitakazoshiriki
Ligi Kuu Bara kugomea udhamini wa Azam, ikidai Sh100 milioni ambazo
klabu zitapewa kila mwaka kwa miaka mitatu ni ndogo.
Azam Televisheni imekubali kudhamini Ligi Kuu Bara
kwa kurusha ‘live’ mechi zote kwa miaka mitatu. Mkataba huo na Bodi ya
Ligi una thamani ya Sh5.6 bilioni.
Kwa takriban wiki tatu sasa, Yanga imekuwa na
malumbano na televisheni ya Azam ikidai kuwa siyo haki kwa kampuni hiyo
kuonyesha mechi za Ligi Kuu Bara kwani wana timu inayoshiriki ligi hiyo.
Katika hoja nyingine ya msingi kupinga udhamini
huo, uongozi wa Yanga unadai kuwa klabu husika hazikushirikishwa
kikamilifu kujadili na hatimaye kukubali udhamini. Katibu Mkuu wa Yanga,
Lawrence Mwalusako alisema jana kuwa mkutano huo umepangwa kufanyika
kwenye ukumbi wa PTA Agosti 18 na ajenda kuu kujadili haki ambayo Azam
wanatarajia kupewa.
Mwalusako alisema kuwa maandalizi ya mkutano huo
yamekamilika na kuwataka wanachama kufika kwa wingi ili kuweka maazimio
ambayo yatapelekwa Shirikisho la Kandanda nchini (TFF).
“Katiba ya Yanga imewapa fursa wanachama kutoa
uamuzi juu ya masuala mazito kama yaliyojitokeza kwa sasa. Uongozi
umeyaona matatizo kwani yanapingana na utaratibu wa sheria za soka,”
alisema Mwalusako.
“Klabu zimekutana na kufanya mkutano kutupinga
sisi, hii ni ajabu sana, sisi hatujapingana na wao, sisi tumepinga bodi
ya Ligi (TPL) na TFF kwa kusaini mkataba na Azam Televisheni,”
aliongeza.
“Kuna klabu zimeundwa juzi tu, hazijawahi hata
kutwaa ubingwa wa Bara, wameingia kwenye mkumbo wa suala hili bila kujua
athari zake za baadaye. Sisi kama viongozi tunalinda na kutetea
masilahi ya Yanga.”
Wakati huohuo, Yanga leo inacheza mechi ya
kirafiki ya kimataifa kama alama ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu
Bara. Mchezo huo dhidi ya timu ya 3 Pillars ya Nigeria utachezwa kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya
ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya timu nyingine ya Ligi Kuu, Mtibwa Sugar
kwenye uwanja huohuo mwanzoni mwa wiki hii.
Chanzo: www.mwananchi.co.tz
Chanzo: www.mwananchi.co.tz




0 comments:
Chapisha Maoni