Wayne Rooney hatasafiri na Manchester United kwenda Sweden leo kwa ajili ya mechi za kiraifiki za kujiandaa kuanza msimu kwasababu ya majeraha ya bega.
United leo imethibitisha kwamba imekataa ofa nyingine ya Chelsea kwa ajili ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 27, vile vile hatakuwepo kwenye mchezo wa kirafiki utakaochezwa na Manchester United dhidi ya AIK Stockholm.
Msemaji wa United amesema kwamba Rooney aliumia bega kwenye mechi iliyochezwa jumamosi dhidi ya Real Betis.
Meneja wa United David Moyes amesema majeraha hayakuwa makubwa, na anaamini Rooney ataweza kurudi mapema kwenye hali yake.
"Wayne ameumia bega kwenye mchezo uliopigwa Jumamosi," Moyes alisema kupitia tovuti ya Klabu. " Hajaumia sana, naamini hatachukua muda kupona.
"Najisikia vibaya atakosa mchezo huu kwasababu nilitaka awe tayari kucheza."
Mapema leo Manchester United imethibitisha kwamba wamekataa ofa ya Chelsea kiasi cha pauni milioni 25.
Msemaji wa Man U alikiambia chombo cha habari cha Press Association Sport: "Tulipokea ofa toka Chelsea jana na tumeikataa muda huo huo. Msimamo wetu ni ule ule, Rooney hauzwi."
Bosi wa Chelsea Jose Mourinho alimpatia kipaumbele cha usajili Rooney, na inakumbukwa kwamba msimu uliopita Rooney alimwambia meneja wake Sir Alex Ferguson kwamba anataka kuondoka Old Trafford.
Moyes amerudia mara kadhaa kwamba Rooney hauzwi. Rooney hakufurahishwa na kauli za meneja wake baada ya kuweka bayana kwamba mshambuliaji Robin van Persie ndiye chaguo lake la kwanza.
Kikosi: Lindegaard, Amos; Rafael, Evans, Evra, Jones, Smalling, Vidic; Anderson, Bebe, Carrick, Giggs, Nani, Zaha; Henriquez, Kagawa, Van Persie, Welbeck




0 comments:
Chapisha Maoni