Mbwatukaji José Mourinho, jana alibwata akisema, wachezaji wa timu ya Chelsea hawajabalehe, amejiuliza endapo wachezaji hao wataweza kukabiliana na mikikimikiki ya UEFA baada ya kushuhudia timu yake ikinyongwa na Basel kikiwa ni kipigo cha kwanza nyumbani katika hatua ya makundi kwa takribani muongo mmoja.
Basel ambayo haijawahi kamwe kupata ushindi katika kiwanja chochote cha Uingereza, jana ilifanikiwa kuifedhehesha Chelsea kwa mabao 2-1 yaliyofungwa dakika 19 za mwisho wa mchezo, na kuwafanya vijana hao wa Mourinho kupoteza mchezo wao wa kwanza wa UEFA Champions wa msimu wa 2013-14. Mmiliki wa timu Roman Abramovich alikuwa uwanjani akishuhudia timu yake ikisulubishwa na Mourinho akiwa ameduwaa baada ya wachezaji wake kushindwa kujitetea wakiwa nyumbani, Darajani.
"Kusema kweli [inaumiza] lakini nadhani timu haijabalehe, haijawa na viwango vizuri vya kuhimili mechi ngumu kama hivi” alisema Mreno huyo, ambaye timu yake imecheza michezo minne bila ushindi ikiwa ni pamoja na mechi waliyopoteza dhidi ya Everton Jumamosi iliyopita.
"Timu ilianza kwa ari ikiwa inatambua majukumu yake, tulitengeneza nafasi nzuri na kucheza kwa kujiamini, lakini wapinzani waliposawazisha, timu ilipata mtikisiko kidogo. Lakini tunaloweza kufanya ni kusahihisha makosa yetu. Tunakwenda nyumbani tukiwa na majonzi, mashabiki nao wana majonzi pia, lakini kesho tunarudi uwanjani kufanya mazoezi kujiandaa na mechi inayofuata. Ninachoamini kwenye soka ni kufanya jitihada, amini kile unachotenda, kuamini wenzako katika mchezo, kujaribu kuondoa tofauti kati yetu, kuwa kitu kimoja na kujitahidi kupata matokeo mazuri dhidi ya Fulham Jumamosi ijayo, ndilo litakaloamsha tabasamu kwa timu na mashabiki kwa ujumla.”
Wakati Romelu Lukaku akiwa ameruhusiwa kujiunga na Everton kwa mkopo, Samuel Eto'o amekuwa akijitahidi kuonyesha uhai katika kikosi baada ya kujiunga na timu hiyo akitokea Anzhi Makhachkala, Fernando Torres hakujumuishwa kikosini, Demba Ba aliyekuwa karibu kujiunga na Arsenal mwezi uliopita aliingia dakika za mwisho.
Meneja huyo alitetea uamuzi wake wa kumruhusu Lukaku kuondoka akidai kuwa nyota huyo alifurahi kuondoka Chelsea kuichezea Everton kwa mkopo. "Tunapopoteza mechi, sizungumzii wachezaji, Wala sizungumzii mtu mmoja mmoja," Alisema Mourinho. "Nazungumzia majukumu yangu na ninafuraha kuwa na mastraika hawa watatu nilio nao msimu huu. Ni wachezaji wazuri, ni wataalamu kwenye soka pia, wanajitahidi kufanya vizuri kwenye kila mechi wanayoshiriki. Siwezi kulaumu yeyote kati yao watatu, wanajitahidi kufanya kila wawezalo kwa ajili ya timu.”
"Samuel, inawezekana amepungukiwa ushap, lakini si jambo linalonishangaza, unapokuwa sehemu isiyokusukuma kufanya mambo makubwa unapungua uwezo kiasi Fulani, unakosa njaa na hamu ya mafanikio. Sasa hali hiyo imemrudia, anahitaji kufanikiwa na kucheza katika kiwango chake cha awali. Anajishughulisha sana, nilimwona kwenye mechi dhidi ya Everton na leo pia. Nadhani tunapaswa kusubiri kidogo ataleta raha tu. Bado ni mchezaji mzuri.”
"Kumaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi ni jambo ambalo bado hatujakata tamaa: Ni jambo tutakalopigania kwa nguvu zote na tunaamini tutashinda tu. Sijatetereshwa na kipigo cha Basel, Sifurahii matokeo haya pia, badala ya kupiga hatua kwenda mbele tumerudi hatua moja nyuma, lakini tuna mechi tano za kucheza bado. Tunaweza na tutashinda."
"Sasa tunapaswa kupata point sita nyumbani [dhidi ya Schalke na Steaua Bucharest] na kupata point nyingine ugenini. Tunaweza kuifaunga Basel kwao ili kufidia kipigo hiki."
![]() |
| Jose Mourinho akiwa hana amani baada ya kushuhudia timu yake ikizidiwa na Basel, Darajani |
![]() |
| Mashabiki wa Chelsea wakionyesha bango kumtaarifu Mourinho kuwa hawafurahii Juan Mata kusugua benchi. |






0 comments:
Chapisha Maoni