HII sasa ni jeuri ya fedha. Azam FC ina
orodha ya makocha watano inayofanya nao mazungumzo, kati yao Kocha
Mfaransa wa klabu tajiri Afrika, TP Mazembe, Patrice Carteron ndiye
anayesakwa kwa nguvu zote.
Wengine ni makocha waliowahi kuinoa Zambia, Dario
Bonetti na Herve Renard ambaye ndiye aliyeipa Zambia ubingwa wa Afrika
mwaka 2012 na kwa sasa anaionoa FC Sochaux ya Ufaransa.
Wengine ni Diego Gazito aliyeifikisha Mazembe
fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia mwaka 2010 na mkurugenzi wa ufundi wa
sasa wa Mazembe, Lamine Ndiaye.
Makocha hao wote ni wa viwango vya juu na yeyote atakayetua nchini ataweka rekodi ya mshahara.
Habari za uhakika kutoka Azam ni kwamba viongozi
wa Azam sasa wapo katika hatua za mwisho za kukubaliana na Carteron ili
ainoe timu hiyo katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara na Kombe la
Shirikisho Afrika mwakani.
Kocha huyo ndiye anayewafundisha Watanzania Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu katika kikosi cha Mazembe.
Azam inajipa matumaini kumnasa Carteron mwenye
umri wa miaka 43 kutokana na mafanikio anayoyapata akiwa na Mazembe
msimu huu katika Kombe la Shirikisho Afrika na kuifikisha timu hiyo
katika fainali ya michuano hiyo.
Carteron aliyewahi kuichezea kwa mkopo Sunderland
ya England mwaka 2001 akitokea AS Saint-Etienne ya Ufaransa ameifikisha
Mazembe fainali Novemba 23 mwaka huu itacheza na CS Sfaxien ya Tunisia
jijini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika mchezo
wa kwanza na kurudiana wiki mbili baadaye.
Azam inajipanga kuvunja mkataba wa kocha huyo ambaye alijiunga na Mazembe Mei 22 mwaka huu.
Mawasiliano ya Azam na Bonetti, Renard na Gazito kwa sasa yamesimama baada ya nguvu kubwa kuelekezwa kwa Carteron na Ndiaye.
Makocha wengine Dorian Marin wa Romania, Zdravko
Logarusic wa Croatia aliyewahi kuinoa Gor Mahia ya Kenya, Fabio Lopez wa
Italia na Patrick Liewig wameiomba Azam iwape kazi waonyeshe mambo
mzunguko ujao.






0 comments:
Chapisha Maoni